MAKUSUDI YETU

Kusudi la Kituo cha Ujamaa ni kuainisha mifumo ya ukandamizaji na kuisambalatisha mifumo hiyo na mahusiano ya mamlaka zinazowezesha mifumo hiyo kuwepo.

Ingawa kusudi letu la msingi ni kukabiliana na tofauti zilizopo katika nchi yetu, ambayo katika dunia ndiyo yenye tofauti kubwa zaidi kati ya matajiri na maskini, tunatambua pia kwamba Afrika Kusini ina nafasi ya pekee katika bara la Afrika. Ina miundombinu mizuri zaidi na raslimali nyingi ambazo zinaweza kusaidia nchi nyingine katika eneo letu la kusini na bara la Afrika kwa ujumla. Hata hivyo, sekta binafsi (mara nyingi kwa kusaidiwa na serikali) hujaribu kutumia raslimali za Afrika Kusini katika namna ambayo inakandamiza nchi nyingine. Kituo cha Ujamaa, kwa upande wake, kinakusudia kutoa raslimali zake kwa ndugu na dada zetu katika eneo la kusini na zaidi katika maeneo mengine katika bara letu ili kukabili ukoloni wa kiuchumi unaofanywa na biashara za Afrika Kusini.

Ili kuisambalatisha mifumo ya ukandamizaji na mahusiano ya mamlaka zinazowezesha mifumo hiyo kuwepo, kwanza, Kituo cha Ujamaa hufanya uchambuzi yakinifu wa jamii “kuanzia ngazi ya chini”. Kwa maneno mengine, tunaanza kutazama ufahamu wa maisha halisia kwa mtazamo wa watu waliomaskini, tabaka la wafanyakazi, wenye VVU, watu wasio na ajira, walionyanyaswa na kupuuzwa. Hii ni hatua ya kwanza ya muhimu na ya msingi.

Pili, Kituo cha Ujamaa kinafanya kazi kwa ushirikiano na jamii pamona na makanisa ili kufanya uchambuzi wao yakinifu wa jamii. Tunatoa kipaumbele kwa vikundi katika jamii na makanisa kwa sababu vinauwezo wa “kumiliki” mradi. Hata hivyo, kama hakuna vikundi, tutaisaidia jamii kuanzisha mfumo wa vikundi. Jambo hili tumeshalifanya, kwa mfano, kuunda vikundi vya waishio na VVU.

Tatu, Kituo cha Ujamaa kinatumia mbinu ya Tazama-Amua-Tenda (inayotokana na chama cha wafanyakazi makasisi wa Ubelgiji na nyaraka za Paulo Frere) na Mtaala wa Biblia wa Mazingira Halisia (MBMH) kama raslimali ya kuwezesha sauti za vikundi zisikike. Wajibu wetu ni kuwa wawezeshaji wa sauti za wengine. Pamoja na kuwezesha sauti za maskini, tabaka la wafanyakazi, na wanyonge, Kituo cha Ujamaa hutoa raslimalia zake kwa kikundi husika pamoja na kukiwezesha kupata raslimali nyingine kutoka vyanzo vingine, ama vya serikali au mashirika yasiyo ya kiserikali.

Nne, kwa kushirikiana na jamii na makanisa tunaweka mipango ya utekelezaji. Kila warsha ya Kituo cha Ujamaa huishia na mpango kazi. Mpango kazi hutokana na jamii husika ambayo tunafanya kazi nayo, na mpango kazi sharti umilikiwe na wanajamii wenyewe. Hata hivyo, tunaiwesesha jamii na kufanya kazi nayo katika mikakati yote ya utekelezaji, ikiwa ni pamoja na utetezi na ushawishi, mabadiliko ya taasisi na/au mfumo, uwezeshaji, nk.

1. Jamii, Jamii ndiyo mwanzo na lengo la Mtaala wa Biblia wa Mazingira Halisia (MBMH); jamii ndiyo vazi la MBMH; jamii za maskini waliohamasika, tabaka la wafanyakazi, na makundi ya wanyonge ndiyo hatua ya msingi na uhalisia wa msingi wa MBMH; Jamii pia ndiyo lengo kuu la MBMH, kwa kuwa MBMH inachangia kuleta ukombozi katika jamii, utu kamili na uzima tele kwa wote.

2. Yakinifu, MBMH huwezesha uchambuzi ‘yakinifu’ wa nyanja zote za maisha; hasa, MBMH inayakinisha na kufanya uchambuzi wa mtu binafsi, jamii na maandiko ya Biblia, kwa kutumia maswali maalumu na yenye mpangilio, na kwa namna hiyo huandaa mazingira ya kimdahalo kati ya mtazamo makini wa maisha na usomaji yakini wa Biblia.

3. Ushirikiano, MBMH hufanyika katika mazingira ya ushirikiano katika kazi ya jamii na ushirikiano katika ufafanuzi wa Biblia miongoni mwa jamii maskini zilizohamasika, tabaka la wafanyakazi, na wanyonge, na pia wanataaluma watakaomageuzi, na wataalamu wa Biblia na theologia wapenda mabadiliko ya jamii na wanaojihusisha na maisha ya jamii; Ushirikiano huanza na kazi halisi katika mapambano ya maisha halisia; kisha Ushirikiano huendelea na kuhusisha ushirikiano katika kufafanua Biblia na kushiriki pamoja katika ‘kuitenda’ theologia, kuondoka kwenye theologia iliyozoeleka na kuelekea kwenye theologia ya watu na theologia ya kiunabii.

4. Mabadiliko, MBMH hutumia Biblia kama zana na kujenga hoja kwa ajili ya kazi ya kuleta mabadiliko katika jamii; Mabadiliko huhusisha mtu binafsi na jamii, pamoja na kanisa (na dini zote kwa ujumla); lengo kuu la mabadiliko ni kubadilisha muundo na mfumo wa jamii, na njia kuu ya mabadiliko ni geuza itikadi na fikra za kitheologia.

5. Mazingira, MBMH hujikita katika nyanja nyingi za mazingira halisi ya maisha, na hasa nyanja za mifumo na miundo ya maisha halisia; MBMH inatambua kuwa mtu binafsi, jamii, na maandiko ni matokeo ya nyanja hizi za maisha halisia; kipekee, MBMH ni zana inayowezesha kuchambua nyanja za mazingira ya kiuchumi, kisiasa, na kidini; MBMH hutambua kuwa mazingira ya maisha hubadilika.

6. Mapambano, katika MBMH ‘mapambano’ ni dhana ya msingi kijamii na kitheologia; katika MBMH tunatambua kuwa mapambano ni sehemu ya mazingira ya maisha halisia, na kwa hiyo katika MBMH tumechagua kusimama upande wa Mungu wa uzima dhidi ya miungu wa mauti; kwenye MBMH ‘uwanja’ mkuu wa mapambano ni itikadi na theologia; MBMH inatambua utata uliyopo katika usomaji wa biblia yenyewe, ikiwa ni pamoja na theologia za kibiblia zinazoleta uzima na theologia za kibiblia zinazoleta mauti; MBMH ‘hugombana’ na maandiko ya biblia ili kuleta uzima.
Contact Webmaster | View the Promotion of Access to Information Act | View our Privacy Policy
© University of KwaZulu-Natal: All Rights Reserved