HISTORIA

Kituo cha Ujamaa kilianza wakati wa mgogoro mkubwa katika jimbo la KwaZulu-Natal Afrika Kusini. Jamii maskini, wafanyakazi na watu wanyonge wa Africa Kusini walisambalatishwa kwa ukatili uliyoungwa mkono na serikali. Katika hali hii ya vifo na ukatili wa kila siku kilio kilisikika, “Tunawezaje kumsikia Mungu akinena nasi katika nyakati hizi?”

Kilio hiki kilikuwa cha kawaida Afrika Kusini wakati wa ubaguzi wa rangi. Serikali ya kibaguzi ilijidai kuwa ni serikali ya Kikristo, na ingawa kulikuwa na baadhi ya sauti za unabii kutoka makanisani, bado makanisa mengi yalifuata msimamo usiotoa changamoto kwa dola. Hivyo basi, kilio cha watu weusi wengi wa Afrika Kusini, wengi wao wakiwa Wakristo, kilikuwa namna ya kupata njia ya kusoma Biblia ili waweze kumsikia Mungu akisema nao. “Injili” iliyotangazwa na serikali ya kibaguzi pamoja na makanisa mengi haikuwa “habari njema” kwa maskini!

Kituo cha ujamaa kikawa ni jibu mojawapo la kilio hiki. Mgogoro wa KwaZulu-Natal, mwishoni mwa miaka ya 1980, uliwaunganisha wataalamu wa Biblia wanaojihusisha na jamii, wasomi wanamageuzi, na wanajamii waliyogawanyika na kutuwezesha kukutana kila siku. Tulianza kusoma Biblia pamoja, tukizingatia kwa makini mchango wa kila mtu. Kilichotokea ndiyo kile tunachokiita sasa “Mtaala wa Biblia wa Mazingira Halisia”.

Mtaala wa Biblia wa Mazingira Halisia una mikazo sita. Mkazo wa kwanza ni kwamba usomaji wa Biblia huanza na maisha halisia ya maskini, wafanyakazi, na jamii za wanyonge. Umwilisho na maisha ya Yesu vinatupa ushuhuda wa wazi kuhusu upendeleo wa Mungu kwa maskini na wanyonge. Hivyo mapambano yao ya kila siku ya uwepo wao, ukombozi, na maisha ndiyo msingi wa kwanza wa tafakari ya kibiblia. Watu wa kawaida hutiwa nguvu wanapogundua kwamba ni halali kwao kuhusisha uzoefu wa maisha na usomaji wao wa Biblia.



Contact Webmaster | View the Promotion of Access to Information Act | View our Privacy Policy
© University of KwaZulu-Natal: All Rights Reserved