KUHUSU KITUO CHA UJAMAA

Kituo cha Ujamaa kilianzishwa mwaka 1985 kikiwa sehemu ya kitivo cha Theologia cha Chuo Kikuu cha Natal wakati ule (kwa sasa kinafahamika kama UKZN). Hakina itikadi za kisiasa, wala dhehebu, ni Kituo cha Maendeleo ya Jamii na Utafiti ambacho kinasaidia kuwajengea watu uwezo katika nyanja za maendeleo na utawala bora kwa ngazi ya kanisa na jamii kupitia elimu ya Theologia ili kuhakikisha ushiriki kamili wa raia wote katika mabadiliko ya jamii. Hapa utapata Muundo wa Ujamaa.

Kituo cha Ujamaa ni matokeo ya mchakato wa kitheologia katika Theologia ya ukombozi, hasa Theologia ya Watu Weusi ya Afrika Kusini na Theologia ya Mazingira Halisia ya Afrika Kusini. Zaidi sana, Kituo cha Ujamaa kimejikita katika kufanya kazi na jamii maskini, tabaka la wafanyakazi, na wanyonge, kwa kutumia raslimali za kibiblia na kitheologia ili kuleta mabadiliko binafsi na ya jamii.

Dhana na tabia ya vitendo ni kiini cha Kituo cha Ujamaa. Tabia ya kutenda inataka moyo usiokoma wa kujitoa katika duara la theologia ya vitendo inayomtaka mtu kutenda-na-kutafakari tena na tena. Hili ni jambo kuu katika kazi yetu. Tabia ya utendaji ndiyo imewezesha Kituo cha Ujamaa kujibu changamoto za maisha halisia ya Afrika Kusini na mazingira ya kusini mwa Afrika. Tunajitahidi kujihusisha na mazingira yetu kwa uaminifu, kwa kutumia raslimali za kibiblia na kitheologia, na kisha kwa uangalifu (na kwa njia rasmi) kutafakari ambayo tumeyafanya na kwa namna gani tumeyafanya. Kutenda ndiko kunakotufanya tuwepo kwenye jamii na kwenye taaluma pia.


Kituo cha Ujamaa ni muungano wa mashirika mawili, yaani Institute for the Study of the Bible (ISB), ambayo ni Taasisi ya Mtaala wa Biblia, na House of Studies for Worker Ministry, ambayo ni Taasisi ya Mtaala wa Huduma kwa Wafanyakazi. Tumefanya kazi ili kuleta mabadiliko tangu miaka ya 1980, tukifanya kazi yetu katika misingi ya maisha halisia katika mazingira yetu yanayobadilika.

Kwa kuzingatia mazingira yetu ya imani na umuhimi wa Biblia na elimu ya neno la Mungu miongoni mwa watu wetu, Kituo cha Ujamaa kinatoa sauti ya unabii kwa kutumia Biblia na raslimali za kitheologia ili kuleta ukombozi na uzima tele kwa wote (Yohana 10:10). Tunaamini, kama Yesu alivyowafundisha wanafunzi wake, kwamba ufalme wa Mungu sharti uje duniani, kama ulivyo mbinguni (Mathayo 6:9-13). Tunatambua kuwa hakuna hakika Biblia ina nafasi gani

Afrika Kusini (na katika bara lote la Afrika) na kwa hiyo kwa maksudi maalumu tunaitumia Biblia kwa kuzingatia mtazamo wa waliomaskini, tabaka la wafanyakazi, na wanyonge.

Kimsingi tunapambana na mifumo ya uovu inayowanasa watu, kuwanyanyasa na kuwapuuza, ikiwemo: mifumo ya uchumi ambayo inapendelea tabaka la matajiri na kuwaacha watu wengi katika umaskini; mfumo dume ambao unawapa wanaume upendeleo na nguvu na kuwakandamiza wanawake na kuwanyanyasa kijinsia kwa namna mbalimbali. Masalia ya mifumo ya ubaguzi inayowapa upendeleo watu weupe, hasa katika sekta binafsi; mifumo ya ukiritimba inayowawezesha wachache kuwa na mamlaka juu ya wengi; mifumo ya kimila ambayo inawanyanyapaa na kuwabagua walio na VVU na wale wanaoishi kwa matumaini na VVU na UKIMWI; mifumo ya serikali inayoshindwa kuwashirikisha raslimali ya utajiri wa nchi watu waliowahitaji; na mifumo ya kanisa inayoshindwa kutoa sauti ya unabii dhidi ya mifumo iliyotajwa hapo juu.


Contact Webmaster | View the Promotion of Access to Information Act | View our Privacy Policy
© University of KwaZulu-Natal: All Rights Reserved