IDARA ZA UJAMAA

Kila idara ndani ya Kituo cha Ujamaa ina muundo na mipango yake ambayo inajibu mahitaji muhimu ya maisha halisia. Tangu tulipoanza mwaka 1989, tumejitahidi kushughulikia mahitaji ya maisha halisia ya jamii. Kila idara inajihusisha na mambo maalumu yaliyopo katika uchambuzi wetu wa kijamii na kitheologia; hata hivyo, idara zetu zote zinafanyakazi pamoja, zinamshikamano na zina uwiano katika mambo mengi.

Idara zote zifuatazo zinatekeleza lengo kuu la Kituo cha Ujamaa:

Theologia ya Mwili: idara hii ya theologia inayoshughulikia mambo ya jinsia kama vile jinsi ya binadamu, VVU & UKIMWI, ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na ukatili dhidi ya makundi maalumu. Kwa kuwa mfumo dume unatawala jamii na kanisa pia kwa kiasi kikubwa na hivyo kutowezesha nafasi ya mijadala, Kituo cha Ujamaa kinajitahidi kutengeneza mazingira yanayotoa nafasi ya mijadala. Mara nyingi Kituo cha Ujamaa hualikwa kusoma Biblia na kuwezesha mijadala ya makundi ambayo lengo lake la msingi ni kuzungumzia masuala haya. Makundi haya huwa ni ya makanisa na mashirika ya kidini.

Theologia ya Mkate: hutengeneza mazingira ya mijadala kwa njia ya tafakari ya Biblia katika mambo ya uchumi, k.m., Biblia na uumbaji na mgawanyo wa utajiri wa dunia. Tunazingatia mantiki ya kiitikadi na kitheologia, tunapofanya uchambuzi yakinifu wa uchumi wa jamii katika mazingira husika. Theologia hii inalengo la kukabiliana na ‘changamoto tatu’ za ukosefu wa ajira, umaskini na matabaka.

Theologia ya Mazingira: inahusiana na mambo ya mazingira; Kituo cha Ujamaa hushirikiana na jumuiya za kidini katika kupanga semina na mijadala ya kibiblia kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia-nchi na utunzaji wa mazingira. Hapa huwa tunasisitiza umuhimu wa Ardhi na Mazingira pia uhusiano wake na Theologia/Biblia.

Theologia ya Watu: Afrika Kusini kuna ongezeko kubwa la makanisa na huduma za kiroho kwa kasi ambayo haijawahi kutokea. Makundi haya yanaibua theologia mpya na yanatupa maana mpya ya neno kanisa; baadhi ya makundi yanaleta uhai katika kanisa, na mengine hayafanyi hivyo. Kituo cha Ujamaa hufanya kazi na makundi haya kwa lengo la kuisoma kwa upya Biblia kwa pamoja ili kukuza uelewa mpya wa Biblia, na kuinusuru Biblia kutoka kwa watu wanaoitumia kwa agenda zao za ukandamizaji. Theologia ya Watu inasisitiza mambo mema ya kitheologia yanayotokana na maisha ya watu mbalimbali, vikundi vya wanaharakati na Makanisa Asilia ya Afrika.

Theologia ya Umma: katika theologia hii tunafanya kazi na jamii katika masuala ya kanisa na siasa. Ujamaa hutengeneza mazingira yanayotoa nafasi ya kusoma Biblia na makanisa ili kugundua ujumbe wa unabii, ambao unaweza kuenezwa kwa njia ya mimbari kanisani, maombi na mikusanyiko ya hadhara. Kituo cha Ujamaa pia huandaa mazingira ambayo yanawezesha viongozi wa serikali kukutana na viongozi wa kanisa ili kujadiliana kwa uwazi na hata kugundua maeneo ya ushirikiano.




Contact Webmaster | View the Promotion of Access to Information Act | View our Privacy Policy
© University of KwaZulu-Natal: All Rights Reserved